Wednesday, November 28, 2012
CAF YATOA ORODHA YA MAKUNDI YALIYOBAKIA KATIKA TUZO ZA MWAKA HUU.
SHIRIKISHO la Soka barani Afrika-CAF limetoa orodha ya makundi yaliyobakia katika tuzo zinazotolewa na shirikisho hilo kwa mwaka huu ambayo ni timu bora ya soka ya wanaume na wanawake pamoja na tuzo ya mchezaji mwenye kipaji zaidi. Mabingwa wa Afrika Zambia, Ivory Coast ambao wanaongoza kwa ubora barani Afrika, Cape Verde ambao wanashiriki kwa mara ya kwanza michuano ya Mataifa ya Afrika 2013 na Jamhuri ya Afrika ya Kati ndio timu zilizoteuliwa kugombea tuzo ya timu bora ya taifa. Mabingwa wapya wa soka wa Afrika kwa upande wa wanawake Equatorial Guinea, timu ya taifa ya wanawake ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Ghana ambao walinyakuwa medali ya fedha katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka huu, timu ya taifa ya Nigeria maarufu kama Falcon ndio timu zitakazogombea tuzo hizo kwa upande wa wanawake. Katika tuzo ya mchezaji mwenye kipaji zaidi lugha nyingine unaweza kuita Most Promising Talent wachezaji watakaochuana kugombea tuzo hiyo ni pamoja na Mohamed Salah wa Misri, Pape Moussa Konate wa Senegal, na Victor Wanyama wa Kenya. Washindi wa tuzo katika makundi hayo watajulikana Desemba 20 mwaka huu katika sherehe zitakazofanyika jijini Accra, Ghana.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment