MAREKEBISHO VIINGILIO SERENGETI BOYS v CONGO
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limefanya mabadiliko kwa kiingilio cha juu cha mechi ya raundi ya mwisho ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 kati ya Tanzania (Serengeti Boys) na Congo Brazzaville itakayochezwa Jumapili (Novemba 18 mwaka huu). Awali kiingilio cha juu katika mechi hiyo itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni kilikuwa sh. 5,000. Lakini kwa lengo la kuwafanya wadau wa kiingilio hicho kuchangia gharama za mechi hiyo sasa kutakuwa na viingilio vitatu tofauti katika viti vya VIP. Kwa VIP A ambayo ina viti 748 kiingilio kitakuwa sh. 10,000, VIP B inayochukua watazamaji 4,160 kiingilio ni sh. 5,000 wakati VIP C yenye viti 4,060 kiingilio ni sh. 2,000. Kwa sehemu nyingine (viti vya rangi ya chungwa, kijani na bluu) ambavyo jumla yake ni 48,590 kiingilio kitabaki kuwa sh. 1,000. Timu ya Congo Brazzaville kwa taarifa tulizopata awali kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu la Congo (FCF) ilikuwa iwasili jana (Novemba 13 mwaka huu) usiku. Lakini timu hiyo haikutokea na sasa tunatarajia itawasili leo (Novemba 14 mwaka huu) saa 8 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines. Congo itafikia Sapphire Court Hotel. Wakati huo huo, Kamati ya Serengeti Boys itakutana na waandishi wa habari kesho (Novemba 15 mwaka huu). Mkutano huo utafanyika kuanzia saa 5 asubuhi hoteli ya JB Belmont, ukumbi wa Ngorongoro.
No comments:
Post a Comment