Monday, November 19, 2012

TOURE AONGOZA KWA KULIPWA FEDHA NYINGI AFRIKA.

KIUNGO wa kimataifa wa Ivory Coast Yaya Toure ametajwa kama mwanamichezo kutoka Afrika anayelipwa fedha nyingi zaidi katika orodha ya wanamichezo wanaolipwa zaidi duniani iliyotolewa na gazeti la Forbes hivi karibuni. Toure mwenye umri wa miaka 29 anashika namba 73 katika orodha ya wachezaji wanaolipwa zaidi duniani akiwa sambamba na mchezaji wa mpira wa kikapu kutoka Marekani Tim Duncan ambao wote kwa pamoja wanakusanya kiasi cha dola milioni 19.1 kwa mwaka. Kiungo huyo ambaye anacheza katika klabu ya Manchester City na mcheza gofu Ernie Els kutoka Afrika Kusini ndio waafrika pekee katika orodha hiyo ya wanamichezo 100 wanaolipwa zaidi iliyotolewa na gazeti hilo. Toure ambaye ni mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika mwaka 2011 ana mkataba wa miaka mitano na City unaomuwezesha kukusanya kiasi cha dola milioni 16.6 ukijumlisha na dola milioni 2.5 kwa ajili ya matangazo unapata dola milioni 19.1 anazokusanya kwa mwaka. Katika orodha hizo inaongozwa na bondia kutoka Marekani Floyd Mayweather akikusanya kiasi cha dola milioni 85 akifuatiwa na bondia mwingine kutoka Philippines Manny Pacquiao anayekusanya kiasi cha dola milioni 62. Wanamichezo wengine na kiasi wanachokusanya ni pamoja na Tiger Woods dola milioni 54.9, LeBron James dola milioni 53, Roger Federer dola milioni 52.7, Kobe Bryant dola milioni 52.3, Phil Mickelson dola milioni 47.8. Wengine ni David Beckham dola milioni 46, Cristiano Ronaldo dola milioni 42.5 na Peyton Manning dola milioni 42.4 anayefunga orodha ya wanamichezo 10 bora wanaolipwa zaidi duniani.

No comments:

Post a Comment