TIMU za taifa za Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars na Visiwani, Zanzibar Heroes kesho zinatarajia kujitupa uwanjani kwa nyakati tofauti kuwania nafasi ya kucheza fainali ya michuano ya Cecafa Tusker Cup inayofanyika jijini Kampala, Uganda. Zanzibar Heroes ambao wametinga hatua hiyo baada ya kuindoa Burundi kwa changamoto ya mikwaju ya penati 6-5 katika mchezo wa robo fainali itaingia uwanjani kuchuana na timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars ambayo iliiondosha Malawi kwa bao 1-0 lililofungwa na mchezaji wa zamani wa Yanga Mike Baraza. Kwa upande wa Kilimanjaro Stars wao wataingia uwanjani huku wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kuiondosha Rwanda katika michuano hiyo baada ya kuifunga mabao 2-0 yaliyofungwa na nyota wake machachari Amri Kiemba na John Bocco ambaye anashikilia usukani wa kufunga mabao mengi sambamba na Mrisho Ngassa wote wakiwa na mabao matano. Mabingwa watetezi wa michuano hiyo Uganda wametinga katika hatua hiyo baada ya kuifunga timu ngumu ya Ethiopia ambayo itashiriki michuano ya Mataifa ya Afrika mwakani kwa mabao 2-0 hivyo Stars haitakuwa na kazi rahisi katika mchezo wa leo. Kocha wa Stars Kim Poulsen amesema kuwa wamejiandaa vyema kwa ajili ya kuikabili Uganda na wana matumaini ya kutinga hatua ya fainali ya michuano hiyo ingawa alikiri hautakuwa mchezo rahisi. Mchezo wa kwanza utakaoanza unatarajiwa kuwa kati ya Zanzibar Heroes na Harambee Stars majira ya saa 10 za jioni wakati mchezo utakaofuata utachezwa majira ya saa moja usiku.
No comments:
Post a Comment