Tuesday, December 4, 2012

SENEGAL YAKUBALI YAISHE.

SHIRIKISHO la Soka nchini Senegal-FSF limetangaza jijini Dakar jana kuwa hawatakata rufani kufuatia adhabu waliyopewa na Shirikisho la Soka barani Afrika-CAF kufuatia tukio la mchezo wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika 2013. Maofisa wa FSF wamesema ingawa wamepewa nafasi ya kukata rufani kuhusiana na uamuzi wa shirikisho hilo kuufungia Uwanja wa Leopold Sedar Senghor kwa kipindi cha mwaka mmoja wameamua kutokupinga adhabu hiyo. Kamati ya Nidhamu ya CAF pia imelitoza shirikisho hilo faini ya dola 100,000 ambayo inatakiwa kulipwa katika kipindi cha miaka miwili. Adhabu hiyo imekuja kufuatia mashabiki wan chi hiyo kuvuruga mchezo wa marudiano wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika baina ya Senegal na Ivory Coast Octoba 13 mwaka huu katika kipindi cha pili wa Ivory wakiwa wanaongoza kwa mabao 2-0. Tukio lilisababisha mchezo huo kusimamishwa huku baadae CAF ikiamua kuiengua Senegal na kuipa nafasi Ivory Coast kufuzu.

No comments:

Post a Comment