BAADA ya miaka 17 kupita toka alipodaka mpira kwa sarakasi uliopewa jina la mtindo wa ng’e katika mchezo dhidi ya Uingereza ambao hautakuja kusahaulika, golikipa machachari wa kimataifa wa Colombia, Rene Higuita amerudia tena mtindo wa aina hiyo wakati wa mchezo wa hisani uliochezwa nchini India. Higuita mwenye umri wa miaka 46 ambaye amestaafu alikuwa akicheza katika kikosi cha nyota wa India ambacho kilikuwa kikicheza na wachezaji nyota wa zamani wa Brazil katika Uwanja wa Yubabharati. Washindi wa Kombe la Dunia Bebeto, Dunga na Juninho Paulista yalikuwa miongoni mwa majina makubwa katika kikosi cha nyota wa Brazil lakini alikuwa Higuita aliyeiteka hadhara kwa kuonyesha mtindo wake wa ng’e katika udakaji.
Kabla ya mchezo kuanza golikipa huyo mwenye vituko vingi wakati wa enzi zake aliwaahidi mashabiki wa India waliojitokeza uwanjani kuwapa zawadi ikiwa ni kama ishara ya kuwashukuru kwa kuwakaribisha vizuri katika mji huo. Higuita aliokoa mpira kwa sarakasi na kumpa umaarufu mkubwa mpira ambao ulipigwa na mshambuliaji wa zamani wa Uingereza Jamie Redknapp ambaye kwasasa ni mwandishi wa makala wa Sportsmail, katika mchezo uliozikutanisha timu hizo mbili Uwanja wa Wembley mwaka 1995.
No comments:
Post a Comment