Monday, December 10, 2012
SITAWADHARAU BRADFORD - WENGER.
MENEJA wa klabu ya Arsenal amesisitiza kuwa hatabadilisha kikosi chake katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya Bradford City baadae leo, michuano hiyo ikiwa ni nafasi pekee kwa klabu hiyo kukata kiu ya kukosa vikombe kwa muda mrefu. Kikosi cha Wenger ambacho kina ukame wa miaka saba ya kukosa taji lolote wamepangwa na timu hiyo ya daraja la pili katika michuano hiyo huku wao wakipewa nafasi kubwa ya kutinga hatua ya nusu fainali. Kocha huyo ambaye amekuwa akisakamwa na mashabiki kutokana na matokeo yasiyo ridhisha ambayo timu hiyo imekuwa ikiyapata katika michezo ya karibuni amesema hatabadilisha kikosi ambacho alikitumia wakati wa mchezo wa ligi walioshinda mabao 2-0 dhidi ya West Bromwich Albion Jumamosi. Beki wa kulia wa klabu hiyo Bacary Sagna atakosa mchezo huo baada ya kupata majeraha ya kifundo cha mguu lakini anatarajia kumpanga Carl Jenkinson kuziba nafasi ya beki huyo wakati akitarajia pia kumpumzisha Jack Wilshere ambaye hajapona sawasawa baada ya kuwa nje kwa miezi 17. Ushindi dhidi ya West Brom ulimaliza mbio zao za mechi nne bila ya kupata ushindi na kuwafunga midomo mashabiki waliokuwa wakimponda kocha huyo kwa kushindwa kuimarisha kikosi chake pamoja na kukabidhiwa fungu la kutosha.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment