Saturday, January 19, 2013

ILIBAKI KIDOGO NITUNDIKE DALUGA - TEVEZ.

MSHAMBILIAJI wa kimataifa wa Argentina na klabu ya Manchester City, Carlos Tevez amekiri kuwa alikaribia kutundika daruga baada ya kugombana na meneja wa klabu hiyo Roberto Mancini. Tevez mwenye umri wa miaka 28 aligombana na Mancini wakati wa mchezo wa hatua ya makundi ya michuano ya Ligi Mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich msimu uliopita wakati alipokataa kupasha moto misuli kama alivyoamriwa na kocha huyo. Nyota huyo alisimamishwa na kuambiwa kuwa hatacheza tena katika klabu hiyo kitendo ambacho kilipelekea kupoteza ladha ya mchezo wa soka na kufikiria kuachana nao kabisa. Akihojiwa Tevez amesema alikuwa akijifungia mwenyewe chumbani na kulia na kuona kama mkosi baada ya kukorofishana na Mancini pamoja na timu yao ya taifa kutolewa nyumbani katika michuano ya Copa Amerika. Aliendelea kusema kuwa kwasasa yuko sawa na amerejesha ari ya kusakata kabumbu huku akiwa na mahusiano mazuri na Mancini. 

No comments:

Post a Comment