Saturday, January 19, 2013

AUSTRALIA OPEN: SERENA, AZARENKA WATINGA 16 BORA.

MWANADADA nyota katika mchezo wa tenisi Serena Williams amefanikiwa kutinga mzunguko wa nne wa michuano ya wazi ya Australia baada ya kumfunga Ayumi Morita wa Japan kwa 6-1 6-3 katika mchezo uliochezwa leo jijini Melbourne. Katika mchezo huo Williams mwenye umri wa miaka 31 raia wa Marekani hakuonyesha dalili zozote za maumivu katika kifundo chake cha mguu aliyopata katika mchezo wa ufunguzi kwa kucheza kiwango bora na kufanikiwa kumfunga Morita akitumia muda wa dakika 66. Williams anayeshika namba tatu katika orodha za ubora kwa upande wa wanawake atakutana na Maria Kirilenko katika hatua ya 16 bora ya michuano hiyo. Naye mwanadada anayeshika namba moja kwa ubora ambaye pia ndio bingwa mtetezi wa michuano hiyo, Victoria Azarenka alifanikiwa kusonga mbele baada ya kumfunga Jamie Hampton wa Marekani kwa 6-4 4-6 6-2. Azarenka mwenye umri wa miaka 25 raia wa Belarus ilibidi atumie uzoefu wake wote baada ya kufungwa seti ya pili na kufanikiwa kushinda seti ya mwisho na sasa atakutana na aidha Elena Vesnina wa Urusi au Roberta Vinci wa Italia katika hatua ya 16 bora.

No comments:

Post a Comment