Saturday, February 9, 2013

HAYATOU AWATETEA WAAMUZI AFCON.

RAIS wa Shirikisho la Soka barani Afrika-CAF Issa Hayatou amesema kuwa baadhi ya maamuzi yenye utata katika michuano ya Mataifa ya Afrika-Afcon hayapaswi kupunguza sifa ya kiwango cha jumla cha waamuzi wanaochezesha michuano hiyo. Makocha na wachezaji wamechukizwa na kiwango cha waamuzi walichokionyesha katika baadhi ya mechi muhimu kwenye michuano hiyo inayoendelea nchini Afrika Kusini lakini Hayatou anaamini kuwa kwaujumla kiwango cha waamuzi kimepanda tofauti na kipindi cha nyuma. Hayatou amedai kuwa kwa ujumla wameridhika lakini katika baadhi ya mechi kuna makosa ya waamuzi yaliyojitokeza haswa katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Ghana na Burkina Faso na makosa mengine katika mchezo wa makundi kati ya Tunisia na Togo. CAF ilitangaza Alhamisi iliyopita kuwa imemsimamisha mwamuzi kutoka Tunisia Slim Jdedi kwa kusimamia vibaya mchezo huo wa nusu fainali ambapo aliizawadia Ghana penati rahisi huku akikataa penati mbili za wazi za Burkina Faso. Maamuzi mengine ya Jdedi yaliyoleta utata ni kumpa kadi ya pili ya njano winga Jonathan Pitroipa kwa kujirusha kwenye eneo la hatari lakini picha za luninga zilionyesha kuwa mchezaji huyo alifanyiwa madhambi ya wazi na mwamuzi alikuwa katika nafasi nzuri ya kuona tukio hilo.

No comments:

Post a Comment