Saturday, February 16, 2013

TAARIFA KUTOKA TFF LEO.

TENGA AWAASA WALIOENGULIWA KUFUATA TARATIBU
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amewataka waombaji uongozi ambao hawaridhiki na uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi kutafuta haki yao kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo (Februari 16 mwaka huu) mchana, Rais Tenga amesema TFF ni moja ya taasisi ambazo zina utaratibu unaoeleweka kwa wadau wake. “Wote tunafahamu taratibu ambazo tumejiwekea juu ya wagombea wetu wanachaguliwaje. TFF ni moja ya taasisi ambazo zina utaratibu unaoeleweka. Hii ni kuanzia wilayani. Kama kuna tatizo zipo njia za kufuata. “Katika mchakato wa uchaguzi wengine wanafanikiwa, wengine wanaachwa. Wameachwa kwa sababu zilizotolewa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi. Ambaye haridhiki anafuata taratibu tulizojiwekea. Atafute haki yake kwa mujibu wa taratibu,” amesema. Rais Tenga amesisitiza kuwa kikatiba hana uwezo wa kuingilia uamuzi unaofanywa na kamati ambazo ameziunda, kwani utawala bora ni kusimamia kanuni ambapo wanaofanya uamuzi lazima waweke wazi sababu za uamuzi waliofikia.
Amesema ambao hawakubaliani na uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF dhidi yao wana njia tatu za kufuata. Njia hizo ni kuiomba Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ipitie uamuzi iliofanya (review), kuandika Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kuomba liingilie au kwenda Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo (CAS). “Hata ukiweka ngazi nne, mtu akiathirika ataona ameonewa tu. Kwa Katiba yetu hapa (Kamati ya Rufani ya Uchaguzi) ndiyo mwisho. Hakuna chombo kingine. Ukiwaomba FIFA waingilie, watakuja na tutawaeleza mchakato wote ulivyokwenda. Tunapenda kuwahakikishia hawa (waathirika) kuwa kwa maslahi ya mpira wa miguu tutasaidia katika hilo wapate haki,” amesema Rais Tenga na kuongeza kuwa tayari waathirika wawili wa uamuzi wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi wameomba marejeo (review) kwenye kamati hiyo hiyo. Amesema TFF imelazimika kuzungumzia suala hilo kwa sababu limekuwa likizungumzwa kinazi zaidi wakati taratibu ziko wazi, hivyo kwa maslahi ya mpira wa miguu ni vizuri taratibu zikafuatwa.
“Nawaomba washabiki wa mpira wa miguu, tumejenga chombo hiki (TFF) kwa muda mrefu. Bado tunaomba watu watusaidie, kwa hiyo matusi hayawezi kubadili kitu. Tunachowahakikishia ni kuwa, mtu anapoomba msaada tutampa kutafuta haki yake. “Hizi ni kamati huru, lazima ziheshimiwe. Ukianza kuziingilia utakuwa umeua mpira wa miguu. Uongozi ni utumishi, tusionekane tunagombana. Huu si ubunge, mbunge anachaguliwa anakwenda kulipwa mshahara. Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF halipwi mshahara. Tusirudi kwenye matusi, tulishaondoka huko,” amesema. Kuhusu mabadiliko ya Katiba yaliyofanyika kwa njia ya waraka, Rais Tenga amesema yamefanyika kwa mujibu wa taratibu, na haikuwa siri. Maeneo yaliyofanyiwa marekebisho ilikuwa ni lazima, kwani mengi yalikuwa ni maagizo kutoka FIFA na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF). Amesisitiza kuwa mabadiliko hayo yamefuata taratibu na hakuna udanganyifu katika hilo, kwani ridhaa ya kutumia waraka iliombwa, na Mkutano ni watu ambao ndiyo wamepitisha mabadiliko hayo.
“Mkutano Mkuu ni watu, si kikao. Katika dunia ya leo mikutano inafanyika kwa tele conference, si lazima watu wakutane sehemu moja,” amesema na kuongeza kuwa mabadiliko hayo yalipitishwa kwa kura 70 dhidi ya 33 zilizokataa. Kuhusu Kanuni kusainiwa kabla ya Katiba, Rais Tenga amesema tarehe ya kuanza kutumika Katiba ni siku ridhaa ilipopatikana, na si siku mhuri wa Msajili ulipopigwa. Mabadiliko ya Katiba yalipita Desemba 15 mwaka jana, Kanuni zilisainiwa Januari 7 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment