Friday, February 1, 2013

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

KUONA TAIFA STARS, CAMEROON 5,000/-
Kiingilio cha chini kwenye mechi ya FIFA Date kati ya Taifa Stars na Cameroon itakayochezwa Jumatano (Februari 6 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kitakuwa ni sh. 5,000 kwa viti vya kijani. Viti vya bluu ni sh. 7,000 wakati viti vya rangi ya chungwa itakuwa sh. 10,000. Kwa viti vya VIP viingilio ni kama ifuatavyo; VIP C sh. 15,000, VIP B sh. 20,000 na VIP A sh. 30,000.
Tiketi zitaanza kuuzwa siku moja kabla ya mchezo katika vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa Ohia/Samora, kituo cha mafuta OilCom Ubungo, Dar Live Mbagala na kituo cha mafuta Buguruni.

FECAFOOT YATAJA NYOTA WAKE 21, ETO’O NDANI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Cameroon (FECAFOOT) limetaja msafara wake wa watu 36 wakiwemo wachezaji 21 wa timu yao ya Taifa Indomitable Lions) wakiongozwa na nahodha Samuel Et’oo Fils kwa ajili ya mechi dhidi ya Taifa Stars itakayochezwa Jumatano. Kiongozi wa msafara wa timu hiyo itakayoanza kuingia nchini keshokutwa (Februari 3 mwaka huu) ni Mwakilishi wa Serikali ya Cameroon, Dieudone Wassi. Naibu kiongozi wa msafara wa Cameroon itakayofikia hoteli ya New Africa ni Makamu wa Rais wa FECAFOOT, John Ndeh. Mbali ya Et’oo, wachezaji wengine waliomo kwenye msafara huo ni Charles Itandje, Benoit Assou Ekoto, Jehu Rustand Youthe (Union Douala), Fabrice Olinga Essono, Allam Nyam, Bouba Aminou, Benoit Angwa, Herve Tchami, Henri Bedimo, Nicolas Nkoulou, Jean Makoun, Jean Kana Biyick, Joel Matip, Vincent Aboubakar, Alexandre Song, landre Nguemo, Pierre Wome, Jean Nyontcha, Achille Emana na Charles Eloundou. Wengine ni Andre Nguidljol Nlend (Mkurugenzi wa Utawala FECAFOOT), Jean Paul Akono (Kocha Mkuu), Martin Ndtouungou Mpile (Kocha Msaidizi), Jacque Songo’O (Kocha wa makipa), Dk. Baoubakary Sidiki (Daktari wa Timu) na Emmanuel Francis Ambane (Psychologist). Pia wapo Tchonkontey Monkam (Fitness Trainer), Rigobert Song (Meneja wa Timu), Aoudou Mvotoung (Team Security), Fouda pascal Linus (Ofisa Habari FECAFOOT), Boubakar Ndou (Meneja Vifaa), Daniel Tcheuffa Tecky (Physiotherapist), Elias Kalaguem (Physiotherapist) na Justin Addo (Wakala wa Mechi). Wakati huo huo, kikosi cha Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kitaingia kambini kesho jioni (Februari 2 mwaka huu) kwenye hoteli ya Tansoma.

YANGA, MTIBWA SUGAR KAZI KWELIKWELI
Yanga na Mtibwa Sugar zinapambana kesho (Februari 2 mwaka huu) katika moja ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom. Mchezo huo utafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mwamuzi Ronald Swai kutoka Arusha ndiye atakayechezesha mechi hiyo inayotarajiwa kuwa na upinzani mkali, kwani wakati Yanga ikiongoza ligi hiyo, wapinzani wao Mtibwa Sugar katika mechi iliyopita walilala mbele ya Polisi Morogoro ambayo ni ya mwisho katika msimamo wa ligi kwa sasa. Polisi Morogoro itakuwa mwenyeji wa African Lyon kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro wakati Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Mgambo Shooting na Ruvu Shooting inayofundishwa na Charles Boniface Mkwasa. Keshokutwa (Jumapili) kutakuwa na mechi mbili. Simba itaumana na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam huku Tanzania Prisons ikiikabili Coastal Union katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

VILLA SQUAD, MORO UNITED UWANJANI FDL
Villa Squad na Moro United zinaumana kesho (Februari 2 mwaka huu) Uwanja wa Karume, Dar es Salaam katika moja ya mechi za kundi B za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inayoanza mzunguko wa lala salama. Kundi A litakuwa na mechi kati ya Mbeya City na Burkina Faso itakayochezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Majimaji na Kurugenzi katika Uwanja wa Majimaji mjini Songea, na Polisi Iringa dhidi ya Mkamba Rangers kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa. Mechi nyingine ya Kundi B itakuwa Transit Camp na Ndanda itakayochezwa Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani. Kundi C ni Polisi Dodoma na Kanembwa JKT (Uwanja wa Jamhuri, Dodoma), Morani dhidi ya Mwadui (Uwanja wa Kiteto, Manyara), Polisi Mara na Pamba (Uwanja wa Karume, Musoma), Polisi Tabora na Rhino Rangers (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora). Ligi hiyo inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa Machi mwaka huu ambapo mshindi wa kila kundi atapanda daraja kucheza Ligi Kuu msimu ujao.

No comments:

Post a Comment