TIKETI STARS, CAMEROON KUANZA KUUZWA FEB 5
Tiketi kwa ajili ya pambano la kimataifa la kirafiki kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Cameroon (Indomitable Lions) zinaanza kuuzwa kesho (Febaruari 5 mwaka huu) katika vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam. Viingilio katika pambano hilo litakalochezwa Jumatano (Februari 6 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 11 jioni ni sh. 5,000 (viti vya kijani), sh. 7,000 (viti vya bluu), sh. 10,000 (viti vya rangi ya chungwa), sh. 15,000 VIP C, sh. 20,000 VIP B na sh. 30,000 VIP A. Vituo vitakavyouzwa tiketi hizo kuanzia saa 2 asubuhi ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa Samora/Ohio, Oilcom Ubungo, Dar Live Mbagala na kituo cha mafuta Buguruni. Vilevile tiketi zitauzwa uwanjani siku ya mechi, na milango itafunguliwa saa 8 kamili mchana. Wakati huo huo, kundi la kwanza na la pili la wachezaji wa Cameroon tayari limetua jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mechi dhidi ya Tanzania (Taifa Stars) itakayochezwa keshokutwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Cameroon chini ya Kocha Jean Paul Akono itafanya mazoezi kesho saa 11 jioni Uwanja wa Taifa. Nayo Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager yenyewe itafanya mazoezi Uwanja wa Taifa leo saa 11 jioni.
12,984 WASHUHUDIA SIMBA, JKT RUVU ZIKITOKA SARE
Watazamaji 12,984 walikata tiketi kushuhudia mechi ya namba 99 ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa jana (Februari 3 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1. Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 ambapo jumla ya sh. 73,532,000 zilipatikana. Kila klabu ilipata mgawo wa sh. 17,443,752.45 ambapo Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 11,216,745.76. Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 8,869,704.64, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 5,321,822.78, Kamati ya Ligi sh. 5,321,822.78, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,660,911.39 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 2,069,597.75.
UCHAGUZI FRAT SASA KUFANYIKA FEB 14
Uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) uliokwama kufanyika mara mbili, sasa utafanyika Februari 14 mwaka huu mjini Morogoro. Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa FRAT wanatakiwa kufika Morogoro siku moja kabla ya tarehe ya uchaguzi. Pia wapiga kura na wagombea wanatakiwa kulipia ada za uanachama kwa mwaka 2013 kabla ya uchaguzi. Wagombea ni Army Sentimea na Said Nassoro (uenyekiti) wakati wanaoomba nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni Juma Chaponda, Juma Mpuya na Tifika Kambimtoni. Abdallah Mitole, Charles Ndagala na Hamis Kisiwa wanawania ukatibu mkuu, nafasi ya Mhazini inagombewa na Jovin Ndimbo. Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ni Kamwaga Tambwe wakati nafasi ya uwakilishi wanawake yupo Isabela Kapera. Wagombea wa nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Emmanuel Chaula na Samson Mkotya.
No comments:
Post a Comment