Friday, March 8, 2013

MZEE KINESI KUKAIMU NAFASI YA MAKAMU MWENYEKITI SIMBA.

Joseph Itang’are (Mzee Kinesi), Kaimu Makamu Mwenyekiti Simba.
Kama mnavyofahamu, jana wajumbe wawili wa Kamati ya Utendaji ya Simba SC, Makamu Mwenyekiti, Geoffrey Nyange na Zacharia Hans Poppe, walitangaza kujiuzulu nyadhifa zao klabuni. Barua za kujiuzulu kwao tayari zimefika kwa Mwenyekiti na akiona maamuzi hayo yanafaa, ataamua kwa mujibu wa maslahi ya klabu. Kamati ya Utendaji imeshtushwa na kujiuzulu kwa wajumbe hao muhimu. Mchango wao ulikuwa bado unahitajika sana ndani ya klabu. Michango yao ya hali na mali ndani ya klabu katika miaka mitatu iliyopita ilikuwa chachu kubwa ya mafanikio yaliyopatikana. Napenda kuchukua nafasi hii kuwaomba wapenzi na wanachana wa Simba kuwa watulivu katika kipindi hiki. Kamati yenu ya utendaji iko imara na inataka kuwahakikishia washabiki kwamba hali si mbaya kama inavyoonekana. Katika kipindi hiki ambapo Makamu amejiuzulu na Mwenyekiti yupo nje ya nchi kwa matibabu, kamati imeniteua kuwa Kaimu Makamu Mwenyekiti hadi Mwenyekiti atakaporudi. Kwa kuzingatia kwamba bado ligi inaendelea na Simba ina mechi ngumu mbele ya safari, Kamati ya Utendaji imeunda kamati ndogo ifahamikayo kwa jina la Kamati ya Ushindi kwa lengo la kusaidia timu kufanya vizuri. Kamati hiyo inaongozwa na Mama Rahma Al Kharoos al maarufu kwa jina la Malkia wa Nyuki. Lengo kubwa la kuanzisha kamati hii ni kusaidia kufanikisha ushindi kwa Simba katika mechi zilizobaki za Ligi Kuu ya Tanzania. 

MPIRA PESA
Kamati ya Utendaji katika kikao chake kilichofanyika juzi, kilipitisha uamuzi wa kuanza mchakato wa mazungumzo na kundi la MPIRA PESA. Lengo ni kuhakikisha tunaondoa misuguano ya ndani kwa ndani baina yetu ili tuweze kuunganisha nguvu na kuokoa timu yetu.

No comments:

Post a Comment