MCHEZAJI tenisi namba moja duniani kwa upande wa wanawake, Serena Williams anatarajia kujaribu kushinda taji la sita la michuano ya WTA Miami Masters inayoendelea huko nchini Marekani. Katika michuano hiyo ambayo zawadi yake ni kitita cha dola milioni 8.5, Williams anatarajiwa kupambana na Flavia Pennetta katika mzunguko wa pili wa michuano hiyo baada ya mwanadaa huyo anayeshika namba 103 katika orodha za ubora kumfunga Johanna Larson wa Sweden kwa 6-4 6-1. Kama Williams akifanikiwa kutinga mzunguko wa tatu kwa kumfunga Pennetta anaweza kukutana na Yahina Wickmayer wa Ubelgiji au Ayumi Morita wa Japan ambaye alimuondosha Heather Watson wa Uingereza kwa 1-6 7-5 6-4. Williams mwenye umri wa miaka 31 anayeshikilia mataji 15 ya Grand Slam amewahi kushinda michuano ya Miami mwaka 2002, 2003, 2004, 2007 na 2008 huku akifika hatua ya fainali katika michuano ya 1999 na 2009. Dada yake Williams ambaye anashika namba 19 katika orodha za ubora Venus anatarajia kuanza kampeni zake kwa kupambana na Kimiko Date-Krumm wa Japan wakati bingwa mtetezi wa michuano hiyo Agnieszka Radwanska wa Poland anatarajiwa kuanza na Hsieh Su-Wei wa Taiwan.
No comments:
Post a Comment