Saturday, March 2, 2013
TFF YAAMUA KUIANGUKIA SERIKALI.
SAKATA la uchaguzi wa Shirikisho la Soka nchini-TFF limechukua sura mpya baada ya shirikisho hilo kuamua kuiangukia serikali kuhusu tamko lake ililotoa hivi karibuni. Serikali kupitia Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Fenera Mukangara iliamua kuingilia kati sakata hilo kwa kuifuta katiba mpya ya mwaka 2012 iliyokuwa ikitumika katika uchaguzi huo pamoja na kumsimamisha msajili huku akiliamuru shirikisho hilo kutumia katiba ya zamani katika mchakato wake wa uchaguzi. Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao cha kamati hilo, rais wa shirikisho hilo Leodgar Tenga amesema marekebisho ya katiba yaliyofanyika yalikuwa ni halali kwakuwa walifuata taratibu zote zinazofaa. Tenga amesema kabla ya kufanya chochote walienda kwa msajili na baada ya siku 15 walikabidhiwa fomu na msajili ya kuendelea na mchatakato wao hivyo kama kuna makosa yalifanyika kwa msajili haoni kwanini iwaathiri wao. Amesema sio nia ya TFF kubishana na waziri ila wanaamini wakati anatoa tamko hilo hakujua ugumu wa utekelezaji wake na waliomshauri hawakuwa makini kuona madhara yanayoweza kujitokeza huko mbele. Kikao hicho pia kimeamua kutotuma barua Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kuwaelezea mabadiliko hayo kwa hofu ya kufungiwa mpaka watakapokaa na waziri kuangalia uwezekano wa kutafuta suluhu ya suala hilo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment