Wednesday, March 27, 2013

VAN PERSIE AMUACHA CRUYFF SASA AMUWINDA KLUIVERT.

MSHAMBULIAJI nyota wa kimataifa wa Uholanzi na klabu ya Manchester United Robin van Persie amefanikiwa kuipita rekodi ya mabao ya nguli wa soka wa nchi hiyo Johan Cruyff baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 4-0 iliyopata timu yake. Cruyff ambaye anahesabiwa kama mmoja wa wachezaji bora katika historia ya soka nchini humo, alifunga mabao 33 katika mechi 48 za kimataifa alizocheza na rekodi hiyo sasa imepitwa na Van Persie ambaye amefikisha mabao 34. Mshambuliaji huyo sasa amebakisha mabao sita ili kumfikia mshambuliaji nyota wa zamani Patrick Kluivert ambaye aliweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa kipindi chote wa nchi hiyo kwa kufunga mabao 40. Uholanzi sasa inahitaji alama sita zaidi katika mechi zao nne zilizobakia katika kundi D ili kujihakikishia nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014 itakayofanyika nchini Brazil.

No comments:

Post a Comment