Tuesday, April 16, 2013

MAANDALIZI YA KOMBE LA DUNIA 2014 BRAZIL, YAINGIA KWIKWI TENA.

MAANDALIZI ya michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika mwaka ujao nchini Brazil imegonga kizingiti kingine baada ya uwanja uliopo katika mji mkuu wa nchi hiyo kushindwa kufunguliwa mpaka mwezi ujao. Ufunguzi wa Uwanja wa Taifa wa Mane Garrincha, uwanja ambao ndio utakaotumika kwa ajili ya mchezo wa ufunguzi wa michuano ya Kombe la Shirikisho mwaka huu sasa umesogezwa mbele mpaka Mei 18. Uwanja huo ulipo jijini Brasilia ulikuwa umepangwa kufunguliwa Jumapili iliyopita na rais wa nchi hiyo Dilma Rousseff lakini mvua kubwa iliyonyesha iliwazuia mafundi kushindwa kumalizia hatua ya mwisho ya kupanda nyasi. Katibu wa kamati ya maandalizi ya michuano hiyo jijini humo, Claudio Monteiro akaririwa akidai kuwa kila kitu kimeshakamilika kwenye uwanja na kilichobakia ni kupanda nyasi pekee hatua ambayo ilikatishwa kutoka na mvua inayoendelea kunyesha hapo. Ni viwanja vinne pekee kati ya sita ambavyo vitatumika kwa ajili ya michuano ya Kombe la Shirikisho ndivyo vilivyokamilika na kufunguliwa na kumebakia miezi miwili kabla ya ufunguzi wa michuano hiyo huku Uwanja wa Maracana nao ukiwa bado katika matengenezo.

No comments:

Post a Comment