Wednesday, April 17, 2013

MICHO ATIMULIWA RWANDA.

SHIRIKISHO la Soka nchini Rwanda-Ferwafa limemtimua kocha wa timu ya taifa ya ya nchi hiyo, Milutin Sredojovic maarufu kama Micho kufuatia matokeo mabaya ambayo yameiandama timu hiyo kwenye mechi zake za hivi karibuni. Katika taarifa iliyotumwa na katibu mkuu wa Ferwafa, Michel Gasingwa kupitia mtandao imedai kuwa kamati ya utendaji ilifikia uamuzi huo ili kuinusuru timu isiendelee kuboronga katika mechi zake. Kutimuliwa kwa Micho ambaye ni raia wa Serbia kumekuja kufuatia tetesi za hivi karibuni kwamba kocha huyo alikuwa akitaka kibarua cha kuinoa timu ya taifa ya Uganda, The Cranes baada ya kutimuliwa kwa aliyekuwa kocha wa timu hiyo Bobby Williamson. Mbali na tetesi za kuitaka Uganda lakini pia kocha huyo pamoja na Williamson pia walihusishwa na tetesi za kutuma maombi ya kuinoa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars lakini walikosa nafasi hiyo. Mbali na kuinoa Rwanda Micho amewahi kushinda taji la Ligi Kuu nchini Uganda mara mbili, Kombe la Ligi na Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Cecafa akiwa kocha wa klabu ya SC Villa ya Uganda. Pia amewahi kuzifundisha klabu za Orlando Pirates ya Afrika Kusini, St George ya Ethiopia, Yanga ya Tanzania na Al Hilal ya Sudan.

No comments:

Post a Comment