MENEJA wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger anaamini kuwa Manchester United ingeweza kushinda taji la Ligi Kuu nchini Uingereza hata bila ya kuwepo mfungaji wake mahiri Robin van Persie. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uholanzi aliondoka Arsenal na kujiunga na United katika kipindi cha usajili wa majira ya kiangazi na amefunga mabao 24 katika mechi 31 za ligi msimu huu. Pamoja na kiwango bora alichokionyesha nyota huyo msimu huu lakini Wenger amekataa kumpa umuhimu wote yeye na kudai kuwa pengo la alama 13 kati ya United na Manchester City waliokuwa wanawafukuza kwa karibu ni kushuka kwa kiwango cha City. Amesema pamoja na kwamba Van Persie ametoa mchango wake lakini United walikuwa wana uwezo wa kufanya hivyo haswa ikizingatiwa mwaka jana walilikosa taji hilo kwa tofauti ya mabao ya kufungwa na kufunga na kuwaachia ubingwa huo City. Wenger ameongeza kuwa katika kipindi cha muda mfupi ujao watarejea katika ushindani kama ilivyokuwa zamani lakini la muhimu kwasasa ni kumaliza katika nne za juu hilo ndio wanaolipa kipaumbele ili waweze kushiriki Ligi ya Mabingwa barani Ulaya msimu ujao.
No comments:
Post a Comment