Thursday, May 23, 2013

FINKE KOCHA MPYA CAMEROON.

CAMEROON imemteua Volker Finke kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya nchi hiyo huku kazi ya kwanza ya Mjerumani huyo ikiwa ni kuhakikisha timu hiyo inafuzu michuano ya Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil. Finke anachukua nafasi ya kocha wa muda wa timu hiyo Jean-Paul Akono ambaye aliwekwa hapo kuziba nafasi ya Denis Lavagne Septemba mwaka jana baada ya Mfaransa huyo kushindwa kuisaidia timu hiyo kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika 2012 na 2013. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 65 aliwahi kuifundisha klabu ya SC Freiburg kuanzia mwak 1991 mpaka 2007 na atakuwa anafundisha kikosi cha timu ya taifa kwa mara ya kwanza baada ya kutemwa na timu ya Urawa Red Diamonds ya Japan na timu ya Cologne ya nchini kwake. Katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia, Cameroon wako kileleni mwa kundi I wakiwa na alama sita katika mechi tatu walizocheza wakifuatiwa na Libya wenye alama tano, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo-DRC alama nne na Togo alama moja. Kazi yake ya kwanza Finke itakuwa ni kukiongoza kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Ukraine utakaochezwa jijini Kiev Juni 2 mwaka huu kabla ya kuhamishia nguvu zao katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Togo Juni 9, DRC Juni 16 na Libya Septemba 6 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment