Tuesday, May 14, 2013

SHEREHE ZA UBINGWA WA PSG ZAINGIA DOSARI HUKO PARIS.

SHEREHE za klabu ya Paris Saint-Germain kutawadhwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu nchini Ufaransa baada ya kupita miaka 19 ziliingia dosari jana baada ya vurugu kuzuka kati ya mashabiki waliokuwa wakipigana na polisi na kupelekea watu 30 kujeruhiwa na wengine 21 kukamatwa. 
Kamishna wa polisi jijini Paris, Bernard Boucault amesema maofisa watatu wa polisi ni miongoni mwa watu waliojeruhiwa katika tukio hilo ambalo limetoa picha mbaya kwa klabu hiyo kutokana na vurugu za mashabiki wake kwa miaka mingi. Katika taarifa yake klabu hiyo imedai kuwa siku hiyo ilitakiwa iwe siku ya furaha katika jiji la Paris lakini sherehe hizo zimevurugwa na mashabiki wachache wakorofi ambao hawahusiki na mambo ya soka. Kwa mujibu wa Boucault, maofisa wa polisi wapatao 800 walisambazwa mitaa ya mji huo kwa ajili ya kuangalia usalama lakini iliwachukua saa kadhaa kumudu kuwatuliza baada ya mashabiki hao kuamua kurusha mawe katika vioo vya maduka na magari yaliyopo karibu.

No comments:

Post a Comment