Monday, June 10, 2013
BALE ANAWEZA KUVUNJA REKODI KATIKA USAJILI - ZIDANE.
KIUNGO wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa na klabu ya Real Madrid, Zinedine Zidane ambaye kwasasa ni mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo amekiri kuwa watatakiwa kuvunja rekodi ya uhamisho kama watataka kumsajili Gareth Bale. Bale ambaye ni winga wa klabu ya Tottenham Hotspurs ya Uingereza amekuwa akihusishwa na tetesi za kwenda Madrid ambapo kuna taarifa kuwa klabu hiyo imetenga kitita cha paundi milioni 85 kwa ajili yake. Kama uhamisho huo ukifanyika utakuwa umevunja rekodi aliyoweka Cristiano Ronaldo wakati aliposajiliwa kutoka Manchester United kwa ada ya paundi milioni 80 miaka minne iliyopita. Zidane amesema kwa kiwango cha mchezaji huyo alichokionyesha msimu uliopita sio ajabu vilabu vingi kumuwania ndio maana anadhani itakuwa gharama kubwa kupata saini yake. Nyota huyo wa zamani aliendelea kusema kuwa kama klabu yoyote yenye uwezo wa kifedha itahitaji saini ya mchezaji huyo lazima watoe dau kubwa na hata kufikia kuvunja rekodi ili Tottenham waweze kumuachia.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment