NYOTA wa tenisi anayeshika namba moja katika orodha za ubora duniani, Novak Djokovic amerejea katika hali yake ya kawaida baada ya kufiwa na kocha wake wa zamani na kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya wazi ya Ufaransa kwa kumfunga Philipp Kohlschreiber wa Ujarumani. Djokovic raia wa Serbia alimfunga Mjerumani huyo kwa 4-6 6-3 6-4 6-4 na kutinga hatua hiyo ambapo sasa atakwaana na Tommy Haas kutafuta nafasi ya kucheza nusu fainali. Mara baada ya mchezo huo Djokovic alielezea masikitiko yake kwa kumpoteza kocha wake wa zamani Jelena Gencic aliyefariki akiwa na miaka 77 huko nchini kwao Jumapili iliyopita. Mwanamama huyo ndiye aliyemtambulisha Djokovic katika ulimwengu wa tenisi wakati akiwa na miaka sita ambapo nyota huyo amemuelezea kama mama yake wa pili kutokana na mafunzo aliyompatia na kumfanya kuwa mchezaji nyota duniani.
No comments:
Post a Comment