Tuesday, June 18, 2013

KAGAME YAANZA KUTIMUA VUMBI DARFUR.

KINYANG’ANYIRO cha michuano ya Kombe la Kagame inayoandaliwa na Baraza la Michezo kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati-CECAFA inatarajiwa kuanza kutimua vumbi leo katika jimbo la Kordofan Kusini licha ya kuwepo wasiwasi kuhusu hali ya usalama. Kutokana na hali hiyo baadhi ya vilabu viliamua kujitoa wakiwemo mabingwa watetezi wa michuano hiyo Yanga, Simba, Falcon zote za Tanzania na Tusker ya Kenya, wakieleza wasiwasi wa usalama wao haswa katika jimbo la Darfur ambapo kutachezwa baadhi ya mechi. Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye, alikwenda Kordofan jana na kukutana na maofisa kutoka Khartoum waliomuhakikishia kwamba michuano hiyo itaendelea bila ya wasiwasi wowote. Musonye amesema lengo kubwa ya kufanya mashindano hayo katika miji hiyo ambayo hali ya usalama bado inasuasua ni kuonyesha kwamba maisha yanaendelea kama kawaida pamoja na migogoro inayoendelea kwa kipindi cha miaka kadhaa. Baadhi ya raia wengi wa Sudan waliohojiwa kuhusiana na hatua hiyo ya CECAFA nao pia wameonyesha hofu michuano hiyo kuandaliwa katika maeneo korofi nchini humo.

No comments:

Post a Comment