Tuesday, June 18, 2013

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

PONGEZI KWA WASHABIKI KUIUNGA MKONO STARS
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linawashukuru washabiki kwa kujitokeza kwa wingi kwenye mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Taifa Stars na Ivory Coast (The Elephants) iliyochezwa juzi (Jumapili) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mwitikio wa washabiki katika mechi hiyo ilikuwa ni moja ya chachu ya kiwango kilichoonyeshwa na Taifa Stars, kwani walishangilia mwanzo hadi mwisho licha ya kupoteza kwa mabao 4-2. Ni matarajio utakuwepo mwitikio kama huo huo katika mechi ijayo ya Taifa Stars ya michuano ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Nyumbani (CHAN) dhidi ya Uganda (The Cranes) itakayochezwa Dar es Salaam kati ya Julai 12-14 mwaka huu. Stars itaingia tena kambini Julai 4 mwaka huu kujiandaa kwa mechi hiyo.



RWIZA KUHUDHURIA SEMINA YA MAKAMISHNA CAF
Kamishna Alfred Kishongole Rwiza ameteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuhudhuria semina ya makamishna itakayofanyika kuanzia Julai 6-7 mwaka huu katika makao makuu ya shirikisho hilo jijini Cairo, Misri. Semina hiyo inashirikisha baadhi ya makamishna wa CAF walioko kwenye orodha ya makamishna ya shirikisho hilo kwa mwaka 2012-2014. Rwiza ni mmoja wa makamishna wa CAF kutoka Tanzania, na mechi ya mwisho kusimamia ilikuwa ya Kombe la Shirikisho iliyochezwa Mei mwaka huu nchini Msumbiji. CAF tayari imeshamtumia tiketi Rwiza, na anatarajia kuondoka nchini Julai 4 mwaka huu kwenda Cairo kwa ndege ya EgyptAir.



MTANZANIA APEWA ITC ACHEZE YEMEN
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa mchezaji Mtanzania Gossage Mtumwa ili aweze kucheza mpira nchini Yemen. Mtumwa ambaye anatoka katika kituo cha kukuza na kuendeleza vipaji cha Rollingstone cha Arusha aliombewa hati hiyo na Chama cha Mpira wa Miguu cha Yemen (YFA) kwa ajili ya kucheza nchini humo. TFF inamtakia kila la kheri Mtumwa katika safari yake ya Yemen, na ni matarajio yetu kuwa atakuwa balozi mzuri wa Tanzania nchini humo ili wachezaji wengine wa Tanzania nao wapate fursa ya kucheza mpira wa miguu nchini Yemen.



KLABU THAILAND YASAKA WACHEZAJI TANZANIA
Klabu ya Thai Port Football ya Thailand inatafuta wachezaji nchini Tanzania kwa ajili ya kucheza mpira wa miguu nchini humo na katika nchi nyingine barani Ulaya. Kupitia kwa wakala wake, klabu hiyo imetuma taarifa kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ikitaka wachezaji wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 28 kwa ajili ya kuwafanyia majaribio ambapo watakaofuzu watacheza nchini humo na katika klabu nyingine za Ulaya ambazo wana ushirikiano nazo. Wachezaji wenye nia ya kufanya majaribio wanatakiwa kutuma taarifa za wasifu wao (CV) kwa klabu hiyo kwa njia ya emaili, wawe na pasi ya kusafiria pamoja na pasi ya mchezaji (player passport). Wakala atapitia vitu hivyo, na kwa wachezaji atakaowahitaji atawatumia tiketi za ndege na viza kwa ajili ya kwenda kufanya majaribio nchini humo, na watakaofanikiwa kabla ya kusaini nao mikataba watawasiliana na klabu zao nchini (kwa wale wenye klabu).

No comments:

Post a Comment