Tuesday, June 18, 2013
HATUNA HAJA YA KULIPA KISASI - MARCELO.
BEKI wa kushoto wa timu ya taifa ya Brazil, Marcelo amesema kuwa kikosi chao hakitakwenda uwanjani kwa ajili ya kulipiza kisasi kwa Mexico kwenye mechi yao ya pili ya michuano ya Kombe la Shirikisho itakayofanyika Fortaleza. Mara ya mwisho timu kukutana Mexico waliibugiza Brazil kwa mabao 2-1 katika fainali ya soka ya wanaume kwenye michuano ya Olimpiki iliyofanyika London mwaka jana. Kufungwa huko kuliwasononesha Brazil ambao hawajawahi kushinda medali ya dhahabu katika michuano hiyo lakini Marcelo amedai kuwa tayari walishahau hayo na sasa wanaangalia kilichopo mbele yao. Marcelo ambaye alikuwa mmoja ya wachezaji watatu waliozidi umri wa miaka 23 kwenye kikosi cha nchi hiyo amesema anakumbuka vyema walipofungwa mchezo huo lakini wameshasahau na sasa wanachotaka ni matokeo mazuri ili waweze kusonga mbele. Brazil ambao ndio wenyeji wa michuano hiyo walianza vyema mchezo wao wa kwanza baada kuifunga Japan kwa mabao 3-0 ambapo leo wanatarajiwa kukwaana na Mexico kabla ya kumalizia mchezo wa mwisho katika kundi A na Italia.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment