Monday, July 15, 2013

ARSENAL YATUA VIETNAM BAADA YA KUFANYA MAUAJI INDONESIA.

BAADA ya kufanya mauaji nchini Indonesia hatimaye kikosi cha Arsenal kikiongozwa na meneja wao Arsene Wenger kimetua nchini Vietnam wakiendelea na ziara yao ya maandalizi ya msimu mpya huko mashariki ya mbali. Wachezaji wa Arsenal wakiwemo Theo Walcott na Wojciech Szczesny waliwasili jijini Hanoi huku wakiwa wamevalia makofia makubwa ya asili ya nchi hiyo na kuopokewa na maelfu ya mashabiki waliokuja kuwalaki katika Uwanja wa Ndege. Ziara yao ya siku tatu waliyofanya jijini Jakarta ilikuwa na mafanikio makubwa baada ya kuimaliza kwa kuitandika bila ya huruma kombaini ya wachezaji nyota wa Indonesia kwa mabao 7-0 hivyo kuweka matumaini ya kikosi hicho kufanya vyema siku za usoni. 
Ushindi huo utakuwa faraja kubwa kwa Arsenal haswa ikizingatiwa kuwa mahasimu wao Manchester United wao walishindwa kutamba katika mechi yao ya kwanza ya kirafiki iliyopigwa huko Bangkok kwa kukubali kipigo cha bao 1-0 chini ya kocha mpya David Moyes. Kwa wa mahasimu wa United, Manchester City wao nao mambo hayakuwaendea vizuri katika ziara yao nchini Afrika Kusini chini ya kocha mpya Manuel Pellegrini baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Super Sport United.

No comments:

Post a Comment