Tuesday, July 2, 2013

MECHI ZA KOMBE LA DUNIA ZITASIMAMISHWA KAMA MABOMU YA MACHOZI YAKIWAATHIRI WACHEZAJI - VALCKE.

KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Jerome Valcke amedai kuwa mechi za Kombe la Dunia mwakani zinaweza kusimamishwa kama mabomu ya machozi kwa ajili ya waandamanaji nje viwanja yataathiri wachezaji. Katika michuano ya Kombe la Shirikisho iliyomalizika Jumapili iliyopita ambayo ndio kama majaribio kabla ya kuanza Kombe la Dunia ilishuhudia vurugu kubwa kati ya waandamanaji wanaopinga serikali na polisi katika baadhi ya viwanja. Valcke amesema FIFA hawana haki ya kuwapangia watu wa usalama na serikali kitu gani cha kufanya, wanachotaka wao ni kuwaomba kuwahakikishia usalama wanaohitaji kwa ajili ya michuano hiyo. Kumekuwa na baadhi ya taarifa kuwa baadhi ya wachezaji wa Brazil waliathirika na mabomu ya machozi yaliyokuwa yakitupwa nje ya uwanja kukabiliana waandamanaji katika mchezo wa fainali uliofanyika katika uwanja wa Maracana jijini Rio de Janeiro. Valcke amesema kama matukio kama hayo yataendelea katika michuano ya mwakani na mmoja kati ya wachezaji 22 kushindwa kucheza kutokana na athari za mabomu hayo mwamuzi hatakuwa na budi bali kusimamisha mchezo.

No comments:

Post a Comment