Tuesday, July 2, 2013

TEKNOLOGIA YA KOMPYUTA KATIKA MSTARI WA GOLI ITATUPA AHUENI KATIKA KOMBE LA DUNIA - WEBB.

MWAMUZI Howard Webb wa Uingereza amedai kuwa waamuzi wana imani kubwa na mfumo mpya wa teknologia ya kompyuta katika mstari wa goli ambao utatumika katika michuano ya Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil. Hakuna bao lolote kati ya mabao 68 yaliyofungwa katika michuano ya Kombe la Shirikisho lililohitaji teknologia hiyo ambayo ndio ilikuwa imeanza kutumika kwa mara ya kwanza kwenye michuano hiyo. Lakini Webb aliwaambia waandishi wa habari jijini Rio de Janeiro kwamba uhakika wa mfumo huo unawapa faida kubwa na waamuzi wana imani kwa kiasi kikubwa na mfumo huo ambao umefungwa na kampuni ya Kijerumani iliyoshinda zabuni hiyo ya GoalControl. Webb amesema hawana shaka na uthabiti wa mfumo huo na umeonekana kufanya kazi vyema hivyo anadhani utaendelea kufanya kazi hata katika michuano ya Kombe la Dunia mwakani. Webb ambaye alichezesha mchezo wa fainali kati ya Kombe la Dunia mwaka 2010 kati ya Hispania na Uholanzi nchini Afrika Kusini ni mmoja katika orodha ya waamuzi 52 ambao watachujwa kwa ajili ya michuano hiyo mwakani.

No comments:

Post a Comment