Monday, July 15, 2013

TUNISIA YAVULIWA UBINGWA WA CHAN NA MOROCCO.

MABINGWA watetezi wa michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani-CHAN, timu ya taifa ya Tunisia wamevuliwa ubingwa rasmi na Morocco katika mechi za kufuzu michuano hiyo zilizochezwa mwishoni mwa wiki. Tunisia walifanikiwa kutoa sare ya bila ya kufungana katika mchezo wao wa ugenini dhidi ya Morocco lakini walijikuta wakifungwa kwa bao 1-0 katika mchezo wa marudiano uliochezwa kwao Jumamosi iliyopita. Kikosi cha Tunisia ambacho kilikuwa kimesheheni nyota kutoka vilabu vya Esperance ambao ni mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Etoile Sahel, CS Sfaxien, Club Africain na CA Bizertin ilitegemewa kusonga mbele katika hatua hiyo lakini bao la mshambuliaji wa Morocco Abdessamad Mbarki katika dakika za majeruhi lilizima ndoto hizo. Michuano hiyo inayoshirikisha timu 16 inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari 11 hadi Februari mosi mwakani nchini Afrika Kusini ambapo Morocco itakuwa ni mara yao ya kwanza kushiriki michuano hiyo. Nchi zingine ambazo zimeshafuzu ni pamoja na Afrika Kusini ambao wamefuzu kama wenyeji huku Ghana na Libya wao nao wakifuzu baada ya wapinzani wao timu za Benin na Algeria kujitoa.

No comments:

Post a Comment