Wednesday, July 10, 2013
WACHEZAJI WA BAYERN WATAWALA ORODHA YA TUZO YA UEFA.
WACHEZAJI wanne wa klabu ya Bayern Munich wameteuliwa katika orodha ya wachezaji 10 na Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA kugombea tuzo ya mchezaji bora wa bara hilo ka msimu wa 2012-2013. Wachezaji hao ni Franck Ribery, Thomas Mueller, Arjen Robben na Bastian Schwainsteiger ambao wote walikuwemo katika kikosi cha Bayern ambacho kilifanikiwa kunyakuwa mataji matatu msimu uliopita. Mbali na hao wengine waliotajwa katika orodha hiyo ni mchezaji bora wa mwaka katika Ligi Kuu nchini Uingereza, Gareth Bale pamoja na mfungaji bora wa ligi hiyo Robin van Persie huku Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wakiwa wachezaji pekee kutoka La Liga ya nchini Hispania kwenye orodha hiyo. Hii itakuwa ni mara ya tatu kufanyika sherehe za tuzo hizo ambapo mwaka 2011 Messi ndiye aliyeshinda huku mchezaji mwenzake wa Barcelona Andres Iniesta akishinda tuzo hiyo mwaka jana. Wachezaji wengine ni Mshambuliaji nyota wa klabu ya Paris Saint-Germain-PSG, Zlatan Ibrahimovic na Robert Lewandowski anayekipiga Borussia Dortmund ambapo orodha ya mwisho ya wachezaji watatu itatajwa Agosti 6 kabla ya sherehe za kumjua mshindi ambazo zitafanyika wakati wa upangaji wa ratiba ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Agosti 29 mwaka huu jijini Monaco.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment