WACHEZAJI Erick Abidal na Samir Nasri wameitwa katika timu ya taifa ya Ufaransa kwa mara kwanza baada ya kupita mwaka katika kikosi cha wachezaji 23 kitakachocheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Ubelgiji jijini Brussels wiki ijayo. Abidal mwenye umri wa miaka 33 alijiunga na Monaco Julai mwaka huu baada ya Barcelona kuamua kutomuongeza mkataba mwingine ambapo mchezo wake wa mwisho akiwa na timu hiyo ilikuwa ni Februari mwaka jana. Beki huyo alikaa nje kwa muda wa miezi 12 baada ya kufanyiwa upasuaji wa kupandikiza ini jingine lakini kocha wa Ufaransa Didier Deschamps amedai kuwa alikuwa akimfuatilia mchezaji huyo katika mechi za kujipima nguvu toka atue Monaco na amejiridhisha kwamba yuko fiti. Nasri mwenye umri wa miaka 26 mara ya mwisho kukipiga katika timu ya taifa ilikuwa katika michuano ya Ulaya mwaka jana, kabla ya kufungiwa kwa mechi tatu kuichezea timu hiyo kufuatia kurushiana maneno na mwandishi katika mchezo wa robo fainali ambao walifungwa na Hispania.

No comments:
Post a Comment