Friday, September 13, 2013

CAPE VERDE YANYANG'ANYWA NAFASI KWA KUTUMIA MCHEZAJI MWENYE KADI.

NDOTO za Cape Verde kupata nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil zilizimika ghafla baada ya Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kuwakuta na hatia ya kutumia mchezaji asiyeruhusiwa katika mojawapo ya mechi zao za kufuzu. Nafasi yao ya kwenda katika hatua ya mtoano inatarajiwa kuchukuliwa na Tunisia ambao walienguliwa mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kupewa kuchapo cha mabao 2-0 wakiwa nyumbani kwao na Cape Verde. Kufuatia kipigo hicho kocha wa Tunisia Nabil Maaloul alijiuzulu wadhifa wake huo kutokana na kipigo hicho cha aibu. Katika taarifa iliyotumwa katika mtandao wake FIFA ilidai kukuta Cape Verde na makosa ya kumchezesha beki wao Fernando Varela ambaye alikuwa akitumikia adhabu baada ya kutolewa nje katika mechi za kufuzu Machi mwaka huu hivyo kuizawadia Tunisia ushindi wa mabao 3-0. Kwa maana hiyo Tunisia inakua imemaliza mechi zake ikiwa inaongoza kundi B na kuungana na washindi wa makundi mengine katika ratiba ya mwisho ya hatua ya mtoano kabla ya timu tano kufuzu kwenda Brazil. Mbali na kuinyima ushindi Cape Verde kamati ya nidhamu ya FIFA pia iliitoza faini nchi hiyo ya dola 6,400.

No comments:

Post a Comment