Thursday, September 19, 2013

MBABE WA MOHAMMAD ALI AFARIKI DUNIA.

BINGWA wa zamani wa ngumi za uzito wa juu, Ken Norton wa Marekani ambaye alimtandika Mohammad Ali amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 70. Norton ambaye afya yake ilianza kuyumba baada ya kupata ugonjwa wa kiharusi na kupooza sehemu kubwa ya mwili wake, amefariki dunia akiwa katika kliniki moja iliyopo jijini Las Vegas, Nevada. Bondia huyo alimvunja Ali taya katika pambano lao walilocheza kwa mara ya kwanza jijini San Diego, California mwaka 1973 ambapo alishinda pambano hilo. Katika pambano lao la mwisho lililofanyika Septemba mwaka 1976 katika Uwanja wa Yankee uliopo jijini New York, Ali alishinda kwa ushindi mwembamba na kurejesha taji lake la uzito wa juu. Norton alianza kucheza ngumi wakati akiwa mwajiriwa wa jeshi la wanamaji nchini Marekani na muda mfupi baadae aliacha shughuli za jeshi na kuingia katika ulimwengu wa ngumi za kulipwa mwaka 1967. Bondia huyo alishinda taji lake la kwanza la uzito wa juu mwaka 1977, na baada ya kustaafu alijishughulisha na mambo ya utangazaji na pia kushirikishwa katika sinema kadhaa.

No comments:

Post a Comment