KIUNGO mahiri wa kimataifa wa Ujerumani, Mesut Ozil amekiri kufurahishwa na uhamisho wake kutoka Real Madrid kwenda Arsenal katika dakika za mwisho kabla ya dirisha la usajili majira ya kiangazi kufungwa jana. Arsenal ilifanikiwa kumnasa nyota huyo kutoka Madrid kwa ada ya euro milioni 50 baada ya nyota huyo kuonyesha nia ya kuondoka Hispania baada ya Gareth Bale kwenda huko. Pia Ozil alionyesha kuchukizwa na kitendo cha kocha wa Madrid Carlo Ancelotti kumuacha katika benchi la wachezaji wa akiba katika mechi dhidi ya Athletic Bilbao ambayo timu hiyo ilishinda kwa mabao 3-1. Ozil mwenye miaka 24 aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa facebook akiwashukuru wale wote waliokuwa nyuma yake katika miaka mitatu aliyokuwepo Madrid na kuwatakia kila la heri huko mbele. Nyota huyo aliendelea kuandika kuwa kwasasa anataka kuelekeza nguvu zake Arsenal ili kuhakikisha anaisaidia kushinda mataji.
No comments:
Post a Comment