NCHI 10 za Afrika ambazo zimetinga hatua ya mtoano ya kufuzu michuano ya Kombe la Dunia mwakani zimejua hatma yao katika ratiba iliyopangwa katika makao makuu ya Shirikisho la Soka barani Afrika-CAF yaliyopo jiji Cairo, Misri. Timu hizo ambazo ni Algeria, Burkina Faso, Cameroon, Ivory Coast, Misri, Ethiopia, Ghana, Nigeria, Senegal na Tunisia ndio zinatafuta nafasi tano za kwenda kushiriki michuano hiyo nchini Brazil. Katika ratiba hiyo Ivory Coast ambao wataanzia nyumbani watakwaana na Senegal, Ethiopia wataikaribisha Nigeria, Tunisia ambao waliingia katika hatua hiyo kwa mlango wa pili wataanza na Cameroon nyumbani. Wengine ni Ghana watakaokwaana na Misri wakati Burkina Faso wenyewe wamepangwa kuchuana na Algeria. Mechi hizo za mtoano zitachezwa kwa mikondo miwili ya nyumbani na ugenini ambapo mechi za mkondo wa kwanza zitachezwa kati ya Octoba 11 na 15 na zile za mkondo wa pili zitachezwa kati ya Novemba 15 na 19 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment