Monday, September 23, 2013

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

PAMBANO LA AZAM, YANGA LAINGIZA MIL 138/-
Pambano la Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya wenyeji Azam na Yanga lililochezwa jana (Septemba 22 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 138,188,000. Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo namba 33 la VPL msimu wa 2013/2014 lililomalizika kwa Azam kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 walikuwa 24,020. Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 33,065,409.1 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 21,079,525.42. Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 16,812,919.89, tiketi sh. 5,022,342, gharama za mechi sh. 10,087,751.93, Kamati ya Ligi sh. 10,087,751.93, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 5,043,875.97 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 3,923,014.64. Mechi iliyopita ya VPL kwenye uwanja huo kati ya Simba na Mbeya City iliingiza sh. 123,971,000.



MECHI YA TOTO, POLISI DOM KUPIGWA J2
Mechi namba 12 ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kati ya Toto Africans na Polisi Dodoma iliyokuwa ichezwe Jumamosi (Septemba 28 mwaka huu) Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza imesogezwa mbele kwa siku moja. Timu hizo za kundi C sasa zitapambana Jumapili (Septemba 29 mwaka huu) kwenye uwanja huo huo ili kupisha mechi namba 10 kati ya Pamba na Stand United FC ya Shinyanga itakayochezwa Jumamosi (Septemba 28 mwaka huu). Mechi nyingine za kundi hilo zitakazochezwa Jumamosi ni Mwadui na Polisi Tabora (Uwanja wa Kambarage, Shinyanga) wakati Kanembwa JKT na Polisi Mara zitacheza kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.

No comments:

Post a Comment