Tuesday, September 3, 2013

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

TAIFA STARS INATAFUTA NAFASI YA PILI - KIM.
KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen amesema wanaipa umuhimu mkubwa mechi ya mwisho ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Gambia kwa lengo ni kuhakikisha wanamaliza wakiwa wa pili katika kundi hilo. Mechi hiyo itachezwa Septemba 7 mwaka huu jijini Banjul, Gambia ambapo Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premiem Lager itaondoka kesho (Septemba 4 mwaka huu) saa 11 alfajiri kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Dakar, Senegal. Kim amesema wanataka kushinda ugenini, kwani licha ya kuwa wameshatolewa lakini ushindi utawaongezea pointi kwa ajili ya viwango (rankings) vya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na pia kuepuka kuanzia ngazi ya awali ya mechi za mchujo za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa fainali za 2015. “Tunacheza mechi hii tukiwa katika mazingira magumu, kwani wengi wa wachezaji wa kikosi cha kwanza ni majeruhi. Sijawahi kukutana na hali hii tangu nilipoanza kuifundisha Taifa Stars, lakini tumejipanga kuhakikisha tunafanya vizuri,” amesema Kim. Amesema kwa mipango ya timu yake mechi hiyo ni muhimu tofauti na wengi wanavyofikiria, na uamuzi wake wa kumwita beki Henry Joseph amezingatia mambo mengi ya kiufundi ikiwemo nafasi anayocheza na uzoefu wa mchezaji aliyekuwa akicheza nchini Norway katika klabu ya Kongsvinger IL. Wachezaji majeruhi katika kikosi hicho ni Shomari Kapombe, Kelvin Yondani, Aggrey Morris, Salum Abubakar, Athuman Idd na John Bocco. Vilevile wachezaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu hawatakuwemo kwenye safari baada ya klabu yao ya TP Mazembe kutuma taarifa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) leo mchana ikidai ni wagonjwa. Wachezaji wanaoondoka kwenda Banjul ni Juma Kaseja, Mwadini Ali, Ali Mustafa, Amri Kiemba, David Luhende, David Mwantika, Erasto Nyoni, Frank Domayo, Haruni Chanongo, Henry Joseph, Jonas Mkude, Juma Liuzio, Khamis Mcha, Mrisho Ngasa, Nadir Haroub, Said Dilunga, Simon Msuva na Vincent Barnabas.


IRINGA YAINYANYASA RUVUMA COPA COCA-COLA
Iringa imeanza kwa kishindo michuano ya Copa Coca-Cola kwa watoto wenye umri chini ya miaka 15 baada ya leo (Septemba 3 mwaka huu) kuitandika Ruvuma mabao 4-0. Hadi mapumziko katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Shule ya Sekondari Iyunga jijini Mbeya, washindi walikuwa mbele kwa mabao 2-0 yaliyofungwa dakika ya 14 na Justin Luvanda huku Alphonce Kalinga akifunga la pili dakika ya 43. Mabao mengine yalifungwa na Juma Rogani katika dakika ya 49 na Luvanda akafumania tena nyavu dakika ya 59. Hiyo ni mechi ya pili mfululizo kwa Ruvuma kupoteza ambapo ya kwanza ililala mbele ya wenyeji Mbeya kwa mabao 3-0.

No comments:

Post a Comment