Thursday, September 5, 2013

WAGENI WANAUA VIPAJI VYA CHIPUKIZI - LIPPI.

KOCHA wa zamani wa timu ya taifa ya Italia, Marcello Lippi amehimiza Ligi Kuu nchini humo maarufu kama Serie A kutokuacha wachezaji chipukizi wa nyumbani na kukimbilia wachezaji wa kigeni ambao wanakuwa na mchango mdogo kwenye timu. Lippi anafikiri kuwa wapo wachezaji wengi kutoka sehemu mbalimbali duniani katika Serie A ambao hawana ubora ukilinganisha na wachezaji chipukizi wa nyumbani na anahofia muendelezo huo unaweza kuathiri soka la Italia katika siku zijazo. Lippi alikaririwa na gazeti moja la michezo nchini humo akidai kuwa hana matatizo na timu kununua wachezaji muhimu wa kigeni lakini kama wananunua mchezaji kwa ajili ya utofauti wa stakabadhi yake ya kusafiria hawezi kuunga mkono hilo. Kocha huyo mkongwe alidai kuwa sio jambo sahihi kuruhusu zaidi ya asilimia 50 ya wachezaji kuwa wa kigeni kwani unawanyima fursa wachezaji chipukizi kung’aa nyumbani kwao. Lippi mwenye umri wa miaka 65 aliiongoza Italia kunyakuwa taji la Kombe la Dunia mwaka 2006 na kwasasa ni kocha wa timu ya Guangzhou Evergrande ya China.

No comments:

Post a Comment