MSHAMBULIAJI mkongwe wa klabu ya Manchester United, Ryan Giggs ameweka rekodi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati timu yake ilipong’ang’aniwa sare ya bao 1-1 na Shakhtar Donetski katika mchezo wa kundi A. Giggs mwenye umri wa miaka 39 aliingia uwanjani katika dakika ya 66 akichukua nafasi ya Marouane Fellaini na kufikisha jumla ya mechi 145 katika michuano hiyo zikiwemo za kufuzu na kumpita mshambuliaji nyota wa zamani wa Hispania Raul. Meneja wa United David Moyes alimpongeza Giggs kwa rekodi hiyo lakini kwa upande mwingine alisononeshwa na matokeo waliyopata baada ya timu yake kuongoza karibu dakika zote za mchezo. Katika mchezo huo United walimkosa Wayne Rooney lakini Robin van Persie alirejea uwanjani na kuipa timu yake bao la kuongoza katika dakika ya 18 kabla ya Shakhtar hawajasawazisha zikiwa zimebaki dakika 14 mpira kumalizika. Baadhi ya matokeo ya mechi zilizochezwa jana ni pamoja na Manchester City walishindwa kutamba mbele ya Bayern Munich kwa kufunguwa mabao 3-1, Bayer Leverkusen waliifunga Real Sociedad kwa mabao 2-1, Paris Saint Germain walishinda mabao 3-0 dhidi ya Benfica. Nyingine ni Juventus iling’ang’aniwa sare ya mabao 2-2 na Galatasaray, Anderlecht walishindwa kutamba mbele ya Olympiacos kwa kufungwa mabao 3-0 na Real Madrid walipata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya FC Copenhagen.
No comments:
Post a Comment