Wednesday, October 23, 2013

USHINDI WA DORTMUND WALIFANYA KUNDI LA ARSENAL KUWA GUMU ZAIDI.

USHINDI wa mabao 2-1 iliyopata timu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani dhidi ya Arsenal katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya jana umepelekea kundi F ambalo linahesabika kama kundi la kifo kuzidi kuwa gumu na lisilotabirika. Katika msimamo kundi hilo sasa Dortmund, Arsenal na Napoli ambao nao waliifunga Marseille kwa mabao 2-1, wote wana alama sita baada ya kushinda michezo miwili na kupoteza mmoja katika michezo mitatu waliyocheza mpaka sasa. Kati ya timu nne katika kundi hilo ni timu mbili pekee ndio zitapata nafasi ya kusonga mbele katika hatua ya timu 16 bora itakapofika Desemba mwaka huu. Mechi zitakazofuata Arsenal itakuwa na kibarua kigumu pale watakapoifuata Dortmund nchini Ujerumani kwa ajili ya mchezo wa maraudiano wakati Marseille watapata nafasi ya kujiuliza pale watakapokuwa wageni wa Napoli, mechi zote zitachezwa Novemba 6 mwaka huu. Katika baadhi mechi zingine za michuano hiyo zilizochezwa jana, AC Milan ilishindwa kuitambia Barcelona katika uwanja wake wa nyumbani baada ya kutoka sare ya bao 1-1, Celtic wakaifunga Ajax Amsterdam kwa mabao 2-1 huku Chelsea wakipata ushindi mnono wa mabao 3-0 ugenini dhidi ya Schalke. 

No comments:

Post a Comment