Tuesday, November 12, 2013

ISHARA YAMPONZA MCHEZAJI WA AL AHLY.

KLABU ya Al Ahly mabingwa wapya wa Africa wamemtosa kikosini mchezaji aliyewapa taji hilo kutokana na siasa za Misri baada ya kuonesha ishara ya kumuunga mkono rais aliyeondolewa madarakani Mohammed Morsi. Al Ahly imesema mchezaji huyo Ahmed Abdul Zaher hatakwenda kwenye michuano ya klabu bingwa ya dunia ya vilabu ya FIFA itakayofanyika mwezi ujao nchini Morocco baada ya kuonyesha ishara ya vidole vinne inayotafsiriwa ni kama ya kumuunga mkono Morsi. Mshambuliaji huyo alifanya ishara hiyo wakati akishangilia goli kwenye ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Orlando Pirates ya Africa Kusini. Morsi rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia kwasasa anakabiliwa na mashtaka ya mauaji kwa waandamanaji wakati wa vurugu zilizotokea Cairo mwaka uliopita. Baada ya kutupia wavuni bao la pili Abdul Zaher alisheherekea kwa ishara hiyo ya vidole vinne inayochukuliwa ni ishara ya kumuunga mkono Morsi ishara inayofahamika kama Rabaa. Akizungumza kuhusu hilo Abdul Zaher amekiri kuonyesha ishara hiyo ya Rabaa, lakini amesema hakuwa na maana yoyote ya kisiasa wala hakuwa na maana ya kuunga mkono upande wowote kikubwa alikuwa anakumbuka vifo vya raia na hata polisi huko Rabaa.

No comments:

Post a Comment