Tuesday, December 3, 2013

BURKINA FASO YAPINGA UAMUZI WA FIFA.

SHIRIKISHO la Soka la Burkina Faso-FBF limekata rufani dhidi ya uamuzi wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA ambao ulitupilia mbali malalamiko yao dhidi ya Algeria kuhusu mechi zao za mtoano za kufuzu Kombe la Dunia 2014. Mwenyekiti wa FBF Sita Sangare aliwaambia waandishi wa habari jijini Ouagadougou kuwa wamenyang’anywa tiketi yao ya kwenda katika michuano hiyo nchini Brazil, wakimtuhumu mwamuzi kwa kuwanyima nafasi hiyo. Sangare amesema kwa tukio la mchezo wa Novemba 19 uliochezwa huko Blida FBF inaweza kudai kuwa nafasi yao ya kwenda Brazil iliporwa kutokana na maamuzi mabovu ya mwamuzi. Sangare aliendeleaa kulalama kuwa bao la Charles Kabore lililokataliwa na muda wa nyongeza uliowekwa bila sababu yoyote ni mfano tosha wa maamuzi mabovu yaliyotokea katika mchezo huo. Wiki iliyopita FIFA ilitupilia mbali malalamiko ya Burkina Faso na kuithibitisha Algeria katika michuano hiyo lakini sasa itabidi ipitie tena rufani hiyo na kutoa uamuzi wake wa mwisho Desemba 5 kabla ya upangwaji wa ratiba Ijumaa hii.

No comments:

Post a Comment