NAHODHA wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi, Ruud Krol amejiuzulu nafasi ya ukocha katika timu ya CS Sfaxien ikiwa zimepita siku chache baada ya kuiwezesha klabu hiyo ya Tunisia kushinda michuano ya Kombe la Shirikisho. Kuondoka kwa kocha huyo mwenye umri wa miaka 64 kunakuja kufuatia kuifundisha timu hiyo kwa miezi 12 yenye mafanikio baada ya kuiwezesha kunyakuwa taji la ligi kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka nane na baadae kuisambaratisha TP Mazembe kwa jumla ya mabao 3-2 katika fainali za mikondo miwili za Kombe la Shirikisho. Krol pia alifanya kazi kama kocha wa muda wa timu ya taifa ya Tunisia wakati ilipocheza mechi mbili za hatua ya mtoano kufuzu Kombe la Dunia ambapo walifungwa kwa jumla ya mabao 4-1. Krol ambaye alikuwa beki enzi enzi zake aliiongoza Uholanzi katika michuano ya Kombe la Dunia 1978 ambapo walifungwa mabao 3-1 na wenyeji Argentina katika mchezo wa fainali.
No comments:
Post a Comment