NGULI wa soka wa Argentina, Diego Maradona ameanza vita vya maneno na Pele kwa kudai kuwa Mbrazil huyo kwa upande wake atabakia mchezaji bora namba mbili. Wawili wamekuwa wakitupiana maneno mara kadhaa kuhusu misimamo yao na Maradona anaonekana hakufurahishwa na Pele kupewa tuzo ya heshima ya Ballon d’Or katika sherehe zilizofanyika jijini Zurich, Switzerland mapema mwezi huu. Maradona ambaye alipewa zawadi kama hiyo katika miaka ya 90 bado anaamini kuwa yeye ndio namba moja na Pele siku zote anamfuata nyuma yake. Maradona aliyekuwa nahodha wa timu ya taifa ya Argentina aliiongoza nchi hiyo kushinda taji la Kombe la Dunia mwaka 1986 na pia kushinda mataji ya ligi katika vilabu vya Barcelona ya Hispania, Napoli ya Italia na Boca Juniors ya nyumbani kwao Argentina. Kwa Pele yeye ameweka historia ambayo haijavunjwa na mchezaji yeyote kwa kunyakuwa mataji matatu ya Kombe la Dunia huku akiwa amefunga mabao 1,283 katika mechi 1,363 alizowahi kucheza.
No comments:
Post a Comment