Wednesday, January 8, 2014

WALCOTT ANAWEZA KUCHEZA KOMBE LA DUNIA - DAKTARI.

DAKTARI bingwa wa upasuaji kutoka Scotland Profesa Gordon Mackay amedai kuwa anaweza kumtibu Theo Walcott na akapona kabla ya kuanza michuano ya Kombe la Dunia Juni mwaka huu. Mackay ambaye alikuwa akifanya kazi katika klabu ya Rangers amesema anaweza kumtibu nyota huyo wa kimataifa wa Uingereza na kurejea uwanjani chini ya miezi minne. Klabu ya Arsenal tayari imemuondoa Walcott katika mipango yake msimu wote pamoja na Kombe la Dunia baada ya kuchanika msuli wa ndani wa goti lake la kushoto katika mchezo dhidi ya Tottenham Hotspurs Jumamosi. Lakini Mackay ametabiri kuwa akitumia kifaa maalumu kinajulikana kwa jina la kitaalamu kama Internal Brace, mchezaji huyo anaweza kuanza kukimbia tena ndani ya wiki 12. Profesa huyo aliendelea kudai kuwa zoezi hilo litahusisha kifaa maalumu atakachokiweka katika goti la mchezaji huyo ambacho kitamsaidia goti lake kutengemaa kwa haraka na kumruhusu kuanza mazoezi mapema. Mackay ambaye amesaidia wanamichezo kadhaa kutokana na utaalamu wake huo anatarajia kuwasiliana na klabu hiyo leo.

No comments:

Post a Comment