MENEJA wa klabu ya Paris Saint-Germain,PSG ya Ufaransa, Laurent Blanc amepata ahueni baada ya wachezaji wake kufanikiwa kukwepa kwenda katika muda wa nyongeza katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya Nantes. Katika mchezo huo kulikuwa na kila dalili ya kuongezwa kwa dakika 30 wakati Olivier Vigneau alipoisawazishiwa Nantes bao baada ya PSG kuongoza kwa kipindi kirefu kwa bao la Zlatan Ibrahimovic. Lakini alikuwa Msweden huyo huyo aliyefunga bao la ushindi katika dakika za mwisho na kuiwezesha PSG kutinga hatua ya fainali ya michuano hiyo ikiwa ni mara yao ya tano. Blanc amesema katika kipindi cha kwanza Nantes waliamua kutocheza na kutumia muda mwingi wakizuia lakini walibadilika kipindi cha pili na kufanikiwa kusawazisha hivyo kufanya mchezo kuwa mgumu zaidi. Kocha huyo alikiri wachezaji wake kuonyesha kuchoka kidogo lakini anashukuru kwa kukwepa kucheza muda wa nyongeza. PSG sasa watakutana na mshindi kati ya Olympique Lyon au Troyes katika mchezo wa fainali.
No comments:
Post a Comment