MSHAMBULIAJI nyota wa zamani wa Zambia, Dennis Lota amefariki dunia jana jijini Johannesburg akiwa na umri wa miaka 40, baada ya kuugua kwa muda mfupi. Lota ambaye alikuwa akifanya kazi kama kocha msaidizi wa klabu ya Moroka Swallows ya Afrika Kusini alijulikana sana kwa umahiri wake wa ufungaji wakati akicheza katika timu ya Orlando Pirates ambako alicheza mechi zaidi ya 100 katika kipindi cha mwaka 1998 hadi 2002. Afrika Kusini ilikuwa kama nyumbani kwao baada ya kutumia muda wake wa uchezaji soka akiwa huko katika vilabu vya Witbank Aces, FC AK, Mpulanga Black Aces na Amazulu huku akicheza kwa kipindi kifupi pia katika vilabu vya FC Sion ya Switzerland na Esperance ya Tunisia. Lota pia aliitumikia timu ya taifa ya Zambia, Chipolopolo huku akiwemo katika kikosi hicho kilichoshiriki fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 1996,1998,2000 na 2002. Aliteuliwa kuwa kocha msaidizi wa Moroka Swallows Machi mwaka 2011 ikiwa ni miaka michache baada ya kutundika daruga. Rais wa Shirikisho la Soka barani Afrika, CAF Issa Hayatou alituma salamu zake za rambirambi kwa familia, Chama cha Soka cha Zambia sambamba na Moroka Swallows na kueleza kusikitishwa na kifo cha nyota huyo.
No comments:
Post a Comment