KLABU ya Real Madrid inatarajiwa kujua hatma ya Cristiano Ronaldo ataongezewa adhabu na Shirikisho la Soka la Hispania, RFEF hapo kesho kufuatiwa nahodha huyo wa kimataifa wa Ureno kutolewa kwa kadi nyekundi Jumapili. RFEF ilitangaza kuwa itakutana ili kujadili adhabu anayostahili Ronaldo Februari 5, siku ambayo Madrid wanakutana na mahasimu wao Atletico Madrid katika mchezo wa Kombe la Mfalme. Nyota huyo wa zamani wa klabu ya Manchester United alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kufuatia kumpiga konzi Carlos Gurpegui wa Athletico Bilbao katika mchezo wa La Liga uliomalizika kwa sare ya bao 1-1. Katika mfumo wa nidhamu wa RFEF, adhabu inaweza kupanda kutoka kufungiwa mechi moja hadi tatu kulingana na kosa lenyewe na ushahidi uliokuwepo. Ronaldo ambaye pia anafikisha miaka 29 hapo kesho amefunga mabao 32 katika mechi 30 alizoichezea Madrid msimu huu.
No comments:
Post a Comment